Back to top

WANAWAKE WAONDOKANA NA KERO YA MAJI MTWARA

03 April 2023
Share

Mradi wa maji uliyojengwa kwa thamani ya zaidi ya shilingi milioni 800, katika Vijiji vya Mwindi na Mbawala, Wilaya Mtwara Vijijini,   umewaondolea kero wanawake wa maeneo hayo waliokuwa wanalazimika kubeba maji kupeleka Zahanati ama kituo cha afya ili waweze kupata huduma ya afya.

Kauli hiyo ya wanawake wa Kijiji cha Mwindi wameitoa baada ya Mwenge wa Uhuru kufungua mradi mkubwa wa maji, uliyojengwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira Vijijini Ruwasa.

Wakizungumza katika ufunguzi huo wanawake hao wamesema kabla ya mradi huo, walikuwa wanalazimika kutafuta maji mabondeni ama kuchimba mashimo ili kutafuta maji ardhini.

Wamesema pale walipokuwa  na wagonjwa hasa wanawake wanaokwenda kujifungua walilazimika kwenda na maji ili yatumike, kuwafanyia usafi kutokana na changamoto ya maji waliyokuwa nayo.

Kwa upande wake Meneja wa Ruwasa mkoa wa Mtwara, Hamisi Mashindika amesema, mradi huo wa zaidi ya shilingi milioni mianane utahudumia wananchi zaidi ya elfu tatu wa vijiji vya mbawala na mwindi.

Kwa upande wake kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa Abdallah Kaim, amewataka wananchi wa Vijiji hivyo kutunza miundombunu hiyo ambayo imegharimu kiasi kikubwa cha fedha.

Hata hivyo ametaka vijana kutumia fursa hiyo ya maji kulima mbogamboga na kufanya ufugaji ili waweze kujiongezea kipato na kusisitiza serikali ya awamu ya sita lengo lake ni kuona kila Kijiji kinapata maji safi na salama.