
Jeshi la Polisi nchini limewaonya baadhi ya watu wachache wanaoendelea kutumia vibaya mitandao ya kijamii na
kusababisha hofu na taharuki kwa wananchi,
Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini Kamisha Msadizi Mwandamizi wa Polisi, SACP, David Misime, amesema onyo hilo linatokana na taarifa iliyorushwa juzi ikionesha gari Land Cruiser Hard Top, ikisombwa na maji, ambapo Mhalifu aliyetengeneza uongo huo aliandika tukio hilo limetokea muda mfupi huko Arusha, ambapo amebainisha kuwa tukio hilo lilitokea mwaka jana nchini Sudan Kusini.
Ameiasa jamii iendelee kuwakumbusha watumiaji wa mitandao ya kijamii, kuwa baadhi ya binadamu wenzao wana magonjwa na wanapopata taarifa za kushtua kama hizo wanaweza kupata madhara makubwa zaidi hata kupoteza maisha.
Amesema Wazazi ambao watashindwa kuwalinda watoto wao, kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha na kusababisha madhara, Jeshi la polisi limesema litawachukulia hatua za kisheria kwa watakaobainika kushindwa kutekeleza wajibu wao.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini SACP, David Misime, amesema kipindi cha mvua, Januari hadi Aprili mwaka huu, kumejitokeza matukio ya watoto kufa maji maeneo mbalimbali hapa nchini ambapo watoto 37 wameripotiwa kufariki dunia.