Back to top

Watu wanne wafungwa miaka 120 jela kwa makosa ya ubakaji.

31 January 2023
Share

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limesema katika kukahakikisha linakomesha vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na watoto limeendelea kushirikisha jamii na kutoa elimu ambapo limebainisha kuwa mkakati waliojiwekea umesaidia jeshi hilo na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka mkoani humo kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wanne na Mahakama kuwakuta na hatia kwa makosa ya ubakaji.

Akitoa taarifa hiyo mapema leo Januari 31,2023 Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishina msaidizi wa Polisi ACP Justine Masejo amewataja waliofikishwa mahakamani kuwa ni James Elirehema, John Sanare, Theophili Salaho, Japhet Mungure ambapo Mahakama hiyo iliwakuta na hatia na iliwahukumu kifungo cha miaka (30) kwenda Jela kila mmoja kwa kosa la ubakaji.

Kamanda Masejo aliendelea kusema kuwa katika kuhakikisha Jeshi hilo linaendelea kufuatilia vitendo vya ukatili wa watoto unaofanywa na baadhi ya watu katika Mkoa huo amesema jeshi hilo lilifanikiwa kumkamata Doreen Lema (30) mkazi wa Baraa katika halmashauri ya jiji la Arusha kwa kosa la kumchoma pasi ya umeme mtoto wake wa kumzaa mwenye umri wa miaka saba katika maeneo mbalimbali ya mwili wake.