Back to top

WAZIRI MKUU MAJALIWA ATOA MAAGIZO KWA AWESO

08 January 2024
Share

Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Maji, Mhe.Jumaa Aweso, kufika katika ofisi za Wakala wa Maji na Usafi Mazingira  Vijijini Mkoa wa Lindi na Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Lindi kufuatilia upungufu uliopo ikiwemo kutotumika kwa gari la uchimbaji visima lililotolewa na Serikali tangu Juni, Pili mwaka jana ili kuwezesha uchimbaji wa visima vya maji.

Ametoa agizo hilo leo, baada ya kufanya ziara katika ofisi za Mamlaka ya  Maji safi na Usafi wa Mazingira Lindi, zilizopo Manispaa ya Lindi na kushuhudia mtambo wa kuchimba visima ukiwa umeegeshwa na hakuna kisima kilichochimbwa tangu ulipotolewa mwaka jana.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu alihoji sababu ya kutotumika kwa pikipiki zilizonunuliwa na Wakala wa Maji na usafi Mazingira Vijijini Mkoa wa Lindi, tangu mwaka 2021 kwa ajili ya kuzigawa kwa jumuiya za watumia maji kwa madai kuwa bado hazijapata usajili.

Akizungumzia kuhusu pikipiki hizo Afisa Manunuzi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Mkoa wa Lindi, Bw.Kenedy Mbwaga amesema kwa muda mrefu wamekuwa wakifuatilia suala la vibali vya kutumia pikipiki hizo kutoka makao Makuu ya  Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira   bila ya mafanikio, ambapo Waziri Mkuu baada ya kupata maelezo hayo amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kupam bana na Kuzuia Rushwa mkoa wa Lindi afuatilie suala hilo.