
Vikundi mbalimbali vinavyotoa huduma za fedha vimetakiwa kusajili vikundi vyao ili viweze kutambulika rasmi na Serikali, ili kupata uhalali wa kisheria na sifa ya kupata mikopo na fursa mbalimbali zinazotolewa.
Wito huo umetolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Nachingwea, Bi. Amina Ally Said, alipokutana na Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha, iliyopo mkoani Lindi kutoa elimu ya masuala ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali.
Amesema ni jukumu la kuhamasisha vikundi kujisajili ili viwe na sifa za kupata mikopo au fursa zozote zinapotokea serikalini kwakuwa vikundi rasmi hupewa kipaumbele.
Aidha, amefafanua kuwa takwimu za vikundi vizijulikana itaisaidia Serikali kupanga mipango na mikakati yake ya kuvifikia vikundi hivyo na kuviwezesha katika mambo mbalimbali ikiwemo mitaji na ushauri wa kitalaam kwa ajili ya kuviendeleza.
