Back to top

NDEJEMBI: WATUMISHI WA ARDHI WASIO WAADILIFU KUCHUKULIWA HATUA

15 August 2024
Share

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Deogratius Ndejembi, amemwelekeza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kumchukulia hatua kali za kinidhamu Afisa Ardhi Mwandamizi Gaudence Mtalo, kwa kusababisha mkanganyiko kwa kukosa uadilifu katika kutekeleza majukumu yake.

Waziri Ndejembi ametoa maelekezo hayo, Jijini Dar es Salaam, wakati wa kikao chake na watumishi wa Ardhi Mkoa wa Dar es salaam na Pwani, baada ya kusikiliza pande mbili zinazodai kumiliki kiwanja kilichopo Tegeta Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, ambacho mtumishi huyo anahusika katika mkanganyiko huo.

Waziri Ndejembi amezitaka pande mbili ambazo zinadai kila mmoja kuwa ni mmiliki wa kiwanja hicho ndugu John Nyoni na Ramadhani Salum Mwikalo, kutoendelea na kazi ya kuendeleza eneo hilo hadi taratibu za kisheria zitakapokamilika na maamuzi yatatolewa na hatua zitazochukuliwa ili kumilikisha kiwanja hicho.

Aidha, Waziri Ndejembi amewataka maafisa ardhi kuwahudumia watanzania wanaofika kwenye ofisi hizo kwa weledi malalamiko ambayo yamekua yakitolewa na wananchi kwa idara za ardhi nchini.

Mhe.Ndejembi pia amemtaka Msajili wa Hati kuongeza kasi ya kuwasikiliza watu hatua itakayosaidia kupata Hati Miliki Ardhi kwa wakati.   

Huo ni mwendelezo wa ziara za Waziri Ndejembi kuijua Wizara hiyo inavyofanyakazi katika sekta ya Ardhi ambayo ndiyo rasilimali inatumika na watu wote wa zote mijini na Vijijini.