Back to top

"TIBA ASILI, TIBA MBADALA ZIJIKITE KWENYE TAFITI" MHAGAMA

26 April 2025
Share

Waziri wa Afya Mhe.Jenista Mhagama, amelitaka Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala nchini, kujikita katika tafiti za dawa za tiba asili na mbadala na kuzitumia tafiti hizo ili zilete mchango kwenye sekta ya Afya.

Waziri Mhagama ameyasema hayo wakati akizindua Baraza jipya la Tiba Asili na Tiba Mbadala Jijini Dodoma, na kwamba ufanyaji wa tafiti hizo na kutoa ushahidi wa kisayansi utasaidia Tanzania kujipambanua ili kutoa wa huduma za tiba asili na tiba mbadala ndani na nje ya nchi.

Waziri Mhagama amelitaka Baraza hilo kusimamia majukumu yake kwa weledi na kudhibiti wanaotaka kukiuka sheria na taratibu za tiba asili na tiba mbadala kwa kuwachukulia hatua stahiki.

Amelielekeza Baraza hilo kuhakikisha linahuisha daftari la wataalam wa tiba asili na tiba mbadala waliosajiliwa na kufanya ukaguzi shirikishi na kuelekezana juu ya umuhimu wa kuwa na leseni hai.

Awali Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe, ameleza kuwa Baraza hilo limekuwa na mafanikio ya kuongeza watoa huduma na kufikia 59,278, vituo 293 na dawa za asili zilizosajiliwa zimeongezeka  na kufikia157.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala Prof. Japhet Otieno, amesema amepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Mhagama na kuahidi kuyafanyia kazi.