
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewahimiza maafisa maendeo ya jamii nchini kushirikiana na kuhakikisha wanashirikishwa katika mipango ya nchi kuanzia ngazi za halmashauri na kuwezesha jamii kujiletea maendeleo endelevu na jumuishi kwa maslahi mapana ya Taifa.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Mei 7, 2025 jijini Dodoma wakati aliposhiriki kwenye Kongamano na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wataalam wa Maendeleo ya Jamii Tanzania.
“Mahali popote ulipo ni muhimu kila mtu ajue upo usisubiri uambiwe upo, ama litokee tatizo ndio waseme nani anaweza, wapeni ulazima wakuu wenu kuwatafuta kupitia chama chenu furukuteni kwenye halmashauri zenu na mahali mlipo,” amesema Dkt. Biteko.
Amewaeleza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kuipa heshima taaluma yao kwa kuunda Wizara maalum ya kushughulikia maendeleo ya jamii. Sambamba na kuongeza idadi ya ajira kwa maafisa hao zaidi ya asilimia 50 katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake.
Ametoa wito kwa Wizara, Serikali za Mitaa, Taasisi, Wakala, Mashirika na Tume nchini kutambua umuhimu wa kada hiyo kwa kushirikiana na maafisa maendeleo ya jamii “ Washirikiane kwenye kupanga maendeleo, wasiachwe nje bali wao ni wakala wa maendeleo,”
Amesema licha ya Maafisa hao kuwa wasajili wa wafanyabiashara wadogo, wasikubali tu kuwa wasajili wa NGO’s, au wasimamizi wa mikopo na kuitwa wakati wa matatizo watu wanaposhindwa kurejesha mikopo badala yake wahakikishe wanashirikishwa pia katika mipango ya maendeleo.
Aidha, Dkt. Biteko amesema katika kuhakikisha kwamba maendeleo yanakuwepo katika ngazi zote za jamii kwa kutumia rasilimali zilizopo na katika kukabiliana na changamoto Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali ikiwemo kuongeza ajira kwa Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii ambapo kwa mwaka mwaka 2022/23 na 2024/2025 Serikali imeajiri jumla ya wataalamu 1500 ili kuboresha utendaji na utoaji huduma bora ngazi ya msingi.
Ametaja baadhi ya jitihada hizo kuwa ni kuanzishwa kwa Mpango wa Taifa wa Kuhamasisha na Kusimamia Maendeleo Ngazi ya Msingi wa Mwaka 2022/23 - 2025/26, Mpango unaolenga kuwafanya wananchi kuwa kitovu cha maendeleo ngazi ya jamii na Taifa. Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) na Fursa mbalimbali za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Mazingira Wezeshi kwa Wadau kuchangia maendeleo.
Jitihada zingine za Serikali ni Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa Mwaka 2024 – 2034, Mkakati unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034. Katika mwaka wa fedha 2024/25 Serikali imetoa ruzuku kwenye mitungi ya gesi ambapo wananchi wananunua mitungi ya gesi kwa nusu ya bei ya kuuzia katika maeneo ya wilayani na vijiji – miji ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Aidha, Dkt.Biteko amesema kuwa Wizara yake itaendelea kushirikiana na maafisa maendeleo ya jamii nchini katika mipango yake ya kusambaza umeme sambamba na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Pamoja na hayo amewataka maafisa hao kuendelea na jukumu lao la kuibua fursa mbalimbali za kiuchumi, kutoa elimu na kuhamasisha jamii kuchangamkia fursa hizo muhimu ikiwemo Fursa ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF), Mikopo ya Asilimia 10 ya Mapato ya Halmashauri kwa Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu na Mikopo ya wafanyabiashara ndogondogo.
“ Ninatambua kuwa moja ya jukumu lenu ni kwamba ninyi ni Wasajili Wasaidizi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri zote nchini. Hivyo ninyi ni kiungo muhimu katika kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali na Mashirika hayo. Nataka nieleze mashirika hayo kuzingatia sheria na taratibu na wachukulieni hatua watakao kiuka,” amesema Dkt. Biteko.
Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Doroth Gwajima amesema kuwa Mkutano huo umehudhuriwa na wadau mbalimbali wa maendeleo ya jamii kutoka sekta ya umma na binafsi wapatao 1,238.
Amesema mafanikio yanayopatikana nchini ni sehemu ya jitihada za maafisa maendeleo ya jamii kwa sababu maafisa hao wametangulia mbele katika kila sekta mfano elimu, ufugaji, afya, mila na utamaduni pamoja na uchumi kwa kubadili fikra na kuhamasisha wananchi ili waweze kushirikiana na Serikali katika mikakati ya maendeleo.
Ametaja lengo la Mkutano huo wa mwaka ni kubadilishana uzoefi na kupeana mbinu za kutekeleza majukumu yao.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Fatma Tawfiq amewapongeza maafisa maendeleo ya jamii kwa kufanya kazi kubwa kwa maslahi ya jamii na Taifa kwa ujumla, aidha Kamati yake itaendelea kuishauri Serikali kutoa fedha za kutosha ili maafisa hao wafanye kazi yao kikamilifu.
Pia, Mhe. Tawifiq amempongeza Rais Samia kwa kuona umuhimu wa kuifanya Wizara ya Mendeleo ya Jamii kujitegemea na ameiomba Serikali kuwapa vitendea kazi maafisa hao mfano magari au pikipiki pamoja na kuiongezea bajeti Wizara hiyo ili maafisa hao waweze kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kwa upande wake, Rais wa Chama Cha Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (CODEPATA), Victor Kabuje amemshukuru Rais Samia kwa kufanya kazi kubwa ya kuwaletea Watanzania maendeleo
Amesema wataalamu wa maendeleo ya jamii wameendelea kuwahimiza na kuhamasisha wananchi wanashiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
“ Sisi kama wataalamu wabobezi wa maendeleo ya jamii tunaendelea kuwa kubadilisha watu fikra na kuhamasisha maendeleo kuanzia ngazi ya familia na jamii, pamoja na kuhimiza wataalamu kuhamasisha wananchi katika matumizi ya nishati safi ya kupikia na tumegawa majiko kwa wananchi katika kila wilaya mfano kwangu nimegawa majiko 280,” amesema Kabuje.