Back to top

PROGRAMU YA CHANJO, UTAMBUZI WA MIFUGO YAZINDULIWA SONGWE

08 July 2025
Share

#HABARI: Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imezindua rasmi programu ya kitaifa ya utoaji wa chanjo na utambuzi wa mifugo kwa Mkoa wa Songwe, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo kwa Mifugo iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa ziara yake mkoani Simiyu. Kupitia programu hiyo, zaidi ya ng’ombe 479,800 na kuku zaidi ya milioni 2.3 wanatarajiwa kunufaika katika Mkoa wa Songwe pekee, ikiwa ni sehemu ya mpango unaotekelezwa nchi nzima.

Uzinduzi wa programu hiyo kimkoa umefanyika ,  katika Kijiji cha Ndanga, Kata ya Mbuyuni, Wilaya ya Songwe, na kuongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dkt. Mhede amesema programu hiyo inalenga kukinga mifugo dhidi ya homa ya mapafu ya Ng’ombe na kwa upande wa kuku ni Kideri, ndui na mafua ambapo chanjo hizo zote  zimepata ruzuku kutoka Serikali ili kuwasaidia wafugaji kupata huduma hiyo.

Dkt. Mhede amefafanua kuwa mpango huo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuongeza thamani ya mazao ya mifugo. Baada ya kupatiwa chanjo na kutambuliwa, wafugaji wataweza kupata mikopo kupitia taasisi za kifedha na kushiriki kwenye biashara ya kimataifa na amesisitiza kuwa mifugo yote itakayochanjwa pia itatambuliwa kwa kuvishwa hereni za kielektroniki ambazo zitasaidia utambuzi wa haraka endapo mnyama atapotea au kuibiwa.

Kwa upande wake, Mshauri wa Mifugo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omary Ayubu Rajabu, amesema kuwa mkoa umeanza kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu umuhimu wa chanjo na utambuzi wa mifugo, pamoja na kushirikiana na viongozi wa wafugaji kufanikisha mpango huo.

Nae Mwenyekiti wa Wafugaji Wilaya ya Songwe, Bw. Lushona Paul Makula, ametoa rai kwa wafugaji wote kutumia fursa hiyo adhimu.

Wafugaji wa eneo hilo wameeleza shukrani zao kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha mpango huo ambao wamesema utakuwa mkombozi kwa mifugo yao. Mzee Mwajuma Doto Bulugu, mkazi wa Ndanga na mfugaji wa ng’ombe 240, amesema kuwa ng’ombe wake wote wamechanjwa na kutambuliwa, na kwamba wanaamini mpango huo utasaidia kukabiliana na magonjwa ya mifugo. Naye Julietha Mwalyehe, mfugaji kutoka Kijiji cha Mbuyuni, amesema kuwa kuku wake wote wamechanjwa bila malipo na ameeleza kuwa msaada huo kutoka kwa Rais Samia ni mkubwa kwa wafugaji.