Back to top

WAFUGAJI KUPATA SOKO LA UHAKIKA LA NGOZI

01 August 2025
Share

Wafugaji sasa wana uhakika wa soko la ngozi inayotokana na mifugo wanayofuga baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kiwanda cha kuchakata ngozi ambacho ni sehemu ya kiwanda cha Kimataifa cha Bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro International Leather-KLIC) kinachoendeshwa kwa ubia kati ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Jeshi la Magereza.

Hayo yalibainishwa katika ziara ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa PSSSF wakiogozwa na Mwenyekiti wao, Bi. Joyce Mapunjo walipotembelea miradi ya Mfuko katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

“Kiwanda hiki cha ngozi ni jibu kwa wafugaji wetu kwani tuna ngozi nyingi sana, hivyo juhudi zifanyike ili kiwanda kiweze kufanya kazi vyema na hatimaye wafugaji wetu wanufaike na mradi huu” alisema Bi. Joyce Mapunjo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa PSSSF.

Ujenzi wa kiwanda cha kuchakata ngozi umekamilika kwa asilimia 100 na kinachoendelea ni majaribio ya mashine na mitambo, hatua ya awali ya uchakataji wa ngozi imeanza kwa majaribio na ifikapo Septemba, 2025 baada ya kukamilisha majaribio  ya mashine, uchakataji wa ngozi utaendelea mpaka hatua ya mwisho. 

Kiwanda kina uwezo wa kuchakata futi za mraba millioni 13 kwa mwaka, ambapo inatarajiwa asilimia 60 zitumike kiwandani na asilimia 40 kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.

Katika kuhakikisha malengo ya kiwanda hicho yanafikiwa, Mwenyekiti wa Bodi alitaka wabia wote wakutane ili kuzitatua changamoto zozote kama zipo ili kiwanda kisonge mbele.

“Kiwanda hiki kikisimamiwa vyema kinaweza kuwa kiwanda cha mfano katika Afrika Mashariki, hivyo hakikisheni kila jambo linakwenda kama ilivyopangwa” alishauri Bi. Mapunjo.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mkugenzi Mkuu wa PSSSF, Dkt. Rhimo Nyasanho alisema, “Tuweke nguvu kwenye kiwanda cha kuchakata ngozi, kwani hapa nchini tuna ngozi nyingi, kwa uwepo wa kiwanda hiki wafugaji wetu watakuwa na soko la uhakika”.

Pia bodi ya wadhamini ilitembelea miradi inayoendeshwa na PSSSF jijini Arusha, ikiwemo mradi wa nyumba za makazi Oloirieni, jengo la kitegauchumi la PSSSF Arusha house na Gold Crest Hotel. 

Mradi wa Oloirieni umefikia malengo ya uwekezaji kwa kurejesha gharama za mradi tangu mwaka 2012 na kuendelea kuwa kitegauchumi muhimu na chanzo cha mapato kwa Mfuko. 

“Nyumba hizi zimekuwa kimbilio la wafanyakazi wa taasisi nyingi za kimataifa zenye makao makuu Jijini Arusha kwani zinaaminika kuwa sehemu salama zaidi na zenye huduma bora.” Amesema Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji PSSSF, Bw. Fortunatus Magambo.

Wajumbe hao wa bodi ya wameridhishwa na usimamizi wa miradi hiyo na kuitaka menejimenti kuhakikisha miradi hiyo inaendelea vyema kama ilivyo sasa.

Awali kabla ya kutembelea miradi bodi ya wadhamini wa PSSSF ilifanya vikao vyake jijini Arusha. Vikiongozwa na Mwenyekiti Bi. Joyce Mapunjo (Mwenyekiti), CPA. Pius Meneno (Makamu Mwenyekiti), Bi. Emma Lyimo, Dkt. Haphsa Hincha, Bw. Tumaini Nyamhokya, Bi. Suzanne Doran, Bi. Vicky Jengo, Bw. Sadi Shemliwa na Dkt. Rhimo Nyansaho (Katibu) ambaye pia Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF.