Back to top

CHAGUENI VIONGOZI WAADILIFU KWA USTAWI WA TAIFA

07 August 2025
Share

Wananchi wameshauriwa kuchagua viongozi waadilifu kwa ustawi na maendeleo ya taifa ,  katika uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Wito huo umetolewa na Kamishna wa Maadili Jaji (Stahiki) Sivangilwa Mwangesi, katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

Mhe. Mwangesi amewasisitiza Watanzania kushiriki katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, na kuongeza kuwa kura zao ni muhimu katika kupata viongozi waadilifu na wenye kujali uzalendo kwanza kwa manufaa ya Taifa letu.

‘’Hakikisheni mnachagua Viongozi wanaojali maslahi mapana ya Taifa na sio wanaotanguliza nafsi zao kwanza na kusahau wananchi ambao wana matarajio makubwa kwao katika kuwaletea maendeleo,’’ alisema Mhe. Mwangesi.

Aidha, Jaji Mwangesi amesema Sekretarieti ya Maadili itashirikiana bega kwa bega na Taasisi zote za elimu katika kuendeleza mradi wa Klabu za Maadili kwenye Taasisi hizo katika kukuza Maadili nchini.

"Tumekuwa na zoezi la kuwajenga wanafunzi kimaadili kwa kuwa na Klabu za Maadili lengo ni kutoa elimu ya maadili wakiwa wadogo na tutaendelea kushirikiana na Taasisi za elimu ili kupata kizazi adilifu kwa Taifa la kesho,” aliongeza.