
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda amekabidhi vitabu vya Elimu ya dini ya Kiislamu kidato cha tano kwa taasisi ya kusimamia ufundishaji wa elimu ya dini ya kiislamu (TISTA).
Makabidhiano hayo yamefanyika katika ofisi za BAKWATA Jijini Dar es Salaam, ambapo Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Mhe. Abubakar Zuberi aliyeambatana na viongozi wengine amepokea vitabu hivyo kwa niaba ya TISTA.
Amesema, Serikali imekabidhi jumla ya nakala 5000 za vitabu vya kiada vya Somo la Elimu ya dini ya Kiislamu vya sekondari kidato cha pili vyenye thamani ya Tsh. 16,000,000 na nakala 1,000 za vitabu vya kiongozi cha mwalimu vyenye thamani ya Tsh. 1,200,000, na kufanya jumla ya vitabu vyenye thamani ya shilingi 17,200,000.
Aidha, Prof. Mkenda amesema, Serikali itavichapa na kusambaza vitabu vya kidato cha sita na vilivyobaki (kidato cha tatu na cha nne) pindi vitakapo kamilika na kuipa BAKWATA nakala kadhaa kwa ajili ya kusambaza katika shule zisizo na umiliki wa Serikali Tanzania Bara na Zanzibar.
Sambamba na hilo Prof. Mkenda ameishukuru TET kwa kuendelea kufanya kazi kwa karibu na TISTA na kuhakikisha inawawezesha kwa kugharamia jukumu zima la uandishi na uidhinishaji wa Vitabu vya Elimu ya Dini ya Kiislamu.
Amesisitiza kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na madhehebu yote ya dini ili kuhakikisha kuwa Elimu ya Dini inafundishwa ipasavyo ili ichangie katika kumjenga mtanzania mwenye maadili mema.
Kwa upande wake Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Mhe. Abubakar Zuberi ameishukuru Serikali kwa ushirikiano uliosaidia katika zoezi la uandaaji wa maudhui ya vitabu vya Elimu ya dini ya kiislamu.
