
Wakulima wa zao la Parachichi nchini wameaswa kuzingatia ubora, ufungashaji na usafirishaji unaokidhi viwango vya kimataifa ili kulifanya zao hilo kuwa shindani katika soko la Dunia na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha Parachichi barani Afrika.
Amesema hayo Mhe. Daniel Chongolo (Mb), Waziri wa Kilimo wakati akifungua Mkutano wa Tatu wa Kitaifa wa Wadau wa Tasnia ya Parachichi Jijini Dodoma. Ameeleza kuwa dhamira ya Serikali ni kuongeza tija ya uzalishaji kutoka tani 6 kwa hekta mwaka 2021 hadi kufikia tani 10.8 kwa hekta mwaka 2030, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Agenda 10/30.
Waziri Chongolo ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) chini ya Mkurugenzi Mkuu Bi. Irene Mlola kuhakikisha inasimamia uongezaji thamani wa Parachichi kwa kuzalisha bidhaa mbalimbali kama mafuta, vipodozi, chakula cha mifugo na bidhaa nyingine. Ametolea mfano na kumpongeza kijana wa Kibondo Farm kwa ubunifu wake wa kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo ‘ice cream’ ya Parachichi.


Aidha, katika kuimarisha zao la Parachichi nchini, Serikali imeanza ujenzi wa vituo 20 vya kukusanyia mazao ya Parachichi na bustani ambao umefikia asilimia 61.1; na kufungua masoko katika nchi za Uholanzi, India, UAE, Ufaransa, Afrika Kusini na China. Hatua hizi zimeongeza uzalishaji kutoka tani 149,340 mwaka 2020/2021 hadi tani 203,473 mwaka 2025/2026, sawa na ongezeko la asilimia 36.24. Mauzo ya nje yameongezeka kwa asilimia 237 na kuingizia Taifa Dola za Marekani milioni 97.2.
Kwa mwaka 2026/2027, Serikali imeahidi kuendelea kutoa mafunzo kwa wakulima 9,500 na maafisa ugani 500, pamoja na kusambaza miche milioni 1.7 kupitia vikundi vya vijana na wanawake.
Mkutano umehudhuriwa na washiriki zaidi ya 400 wakiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo; Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutoka Songwe, Rukwa, Njombe, Mbeya, Kigoma, Kagera, Iringa, Tanga, Arusha, Kilimanjaro, Ruvuma na Dodoma; wakulima, wasindikaji, wafanyabiashara, wasafirishaji na wadau wengine wa mnyororo wa thamani wa Parachichi.

