Back to top

Wakulima wa Mpunga Moshi walalamikia viongozi kwa ubadhilifu

02 September 2018
Share

Wakulima wa Mpunga katika kijiji  cha Rau kata ya Mabogini wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro wamelalamikia viongozi wa skimu ya umwagiliaji maji Rau ufujaji fedha za mradi wa visima  vitatu  unaotekelezwa kwa michango ya wananchi  kwa ajili ya umwagiliaji ili kukabilina na tatizo la uhaba wa maji umwagiliaji wa Mpunga.

Wakulima hao wamesema  viongozi hao wamechangisha fedha kila mkulima shilingi elfu ishirini kwa ajili ya ujenzi wa visima hivyo  bila mafanikio jambo ambalo limewafanya kukosa imani na viongozi hao.

Wamesema mpaka sasa imebainika kuwepo ubadhirifu wa fedha zaidi ya shilingi milioni 5  katika mradi huo na kwamba wanasikitishwa na hatua ya viongozi hao kushindwa  kutoa taarifa ya mapato na matumizi licha ya kutakiwa kufanya hivyo.

Wakitolea ufafanuzi wa tuhuma hizo za ubadhilifu wa fedha mwenyekiti wa kijiji cha Rau Bw.Aloyce Mobumri  na mwenyekiti wa mradi wa skimu ya mpunga Rau Bw.Abrahaman Juma wamekiri kuwepo na mapungufu ya kushindwa kushirikisha wananchi katika zoezi zima  la uchangishaji wa fedha hizo.

Mradi huo wa umwagiliaji katika skimu ya Rau inayotegemea na wakulima wa kijiji hicho unagharimu zaidi ya shilingi milioni 200 na kwamba lengo la ujenzi wa visima hivyo  ni  kukabilina na tatizo la  uhaba wa maji kutokana na ukame ambao unasababisha mpunga kukauka kwa kukosa maji.