Back to top

Mgunduzi wa Madini ya Tanzanite marehemu Jumanne Ngoma azikwa Same.

02 February 2019
Share

Mgunduzi wa madini ya Tanzanite na Madini ya Jasi Marehemu Jumanne Ngoma ambaye alifariki katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam Januari 30,2019, amezikwa katika kijiji cha Makanya wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro

Waziri wa Madini Mh.Dotto Biteko liyeongoza mamia ya waombolezaji  katika mazishi hayo ya mgunduzi wa Madini ya Tinzanite, akitoa salamu za serikali kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli, amesema kwamba marehemu Jumanne Ngoma ameacha ujumbe kwa vizazi vya sasa na vijavyo kwa kuwa Mwaafrika wa kwanza kugundua Madini ya Tanzanite.

Waziri wa Madini Dotto Biteko. 

Aidha Waziri Biteko ameitaka familia na wachimbaji wa Madini ya Tanzanite  kuweka kumbukumbu ya uwepo wa mzee Ngoma kwa vizazi vijavyo kama mgunduzi wa Madini ya Tanzanite pamoja na kuweka msisitizo kwa serikali kumtambua kama mwanzilishi wa madini ya hayo.

Kwa upande wake Shekhe wa msikiti wa Makanya Hamisi Abubakari amesema wanadamu wameumbwa kwa ajili ya kufa na sio kuishi milele ambapo amesema ni jukumu la kila mtu kujiandaa na maisha mapya baada ya kifo.

Akisoma wasifu wa marehemu mzee Jumanne Ngoma mtoto wake wa kike Asha Jumanne amesema mzee ngoma akiwa mdogo aliondoka Makanya na kwenda Mererani  kutafuta maisha akijishughulisha na ufugaji na baadaye kwenda kozi ya miezi mitatu ya Madini ndipo alipoanza harakati za ugunduzi wa Madini ya Tanzanite na Madini ya Jasi.

Safari ya mwisho ya Marehemu Jumanne Ngoma katika kijiji cha Makanya wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro

Marehemu Jumanne Ngoma amefariki akiwa na umri wa miaka 80 baada ya kuugua ugonjwa wa kiharusi mwaka 2018 na kupatiwa matibabu ndani na nje ya nchi , ameacha watoto nane  na wajukuu.

Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema.