Back to top

Rais Magufuli afanya mabadiliko Ilala.

09 August 2020
Share

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Bw. Ng’wilabuzu Ndatwa Ludigija kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mkoani Dar es Salaam.

Kabla ya uteuzi huo, Bw. Ludigija alikuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni Mkoani Dar es Salaam na anachukua nafasi ya Bw. Mussa Ramadhan Chogelo ambaye amepangiwa kazi maalum katika Ofisi ya Rais.

Kufuatia uteuzi huo, Mhe. Rais Magufuli amemhamisha kituo cha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe Mkoani Katavi Bw. Erasto Nehemia Kiwale ambaye anakwenda kuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni Mkoani Dar es Salaam.

Bw. Kiwale anachukua nafasi ya Bw. Ng’wilabuzu Ndatwa Ludigija ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bi. Catherine Michael Mashalla kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe Mkoani Katavi.

Kabla ya uteuzi huo, Bi. Mashalla alikuwa Afisa Elimu wa Manispaa ya Kigamboni Mkoani Dar es Salaam na anachukua nafasi ya Bw. Erasto Nehemia Kiwale ambaye amehamishwa kituo cha kazi na kuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni.