Back to top

Umoja wa Afrika waanza kutumia kiswahili kama lugha ya kazi.

21 April 2022
Share

Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Umoja wa Afrika, Mhe. Balozi Innocent Shiyo, ameipongeza Kamisheni ya Umoja wa Afrika kwa kuanza kutumia Lugha ya Kiswahili kama ya lugha ya kazi ikiwa ni utekelezaji wa Azimio la Mkutano wa 35 wa Wakuu wa Nchi na Serikali la kutumia Kiswahili kama lugha ya Kazi ya Umoja huo lililotolewa mwezi Februari 2022.

Balozi Shiyo ametoa pongezi hizo leo tarehe 21 Aprili 2022, ikiwa ni kwa mara ya kwanza Mkutano wa 71 wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika kuhusu Haki za Binadamu ambao unafanyika mjini Banjul nchini Gambia kuanzia tarehe 21 Aprili 2022 hadi 13 Mei 2022 kutumia Kiswahili kama lugha ya kazi.

Mkutano huo pamoja na mambo mengine utapokea na kujadili taarifa mbalimbali kuhusu hali ya haki za binadamu barani Afrika na kupokea taarifa kutoka kwa Nchi Wanachama, Tume za Haki za Binadamu na Asasi za Kiraia. Vilevile, pamoja na huduma za ukalimani, nyaraka mbalimbali za mkutano huo pia zitapatikana katika lugha ya Kiswahili.

Balozi Shiyo ameeleza kuwa, hatua hii ya kipekee inaifanya Lugha ya Kiswahili kuwa lugha pekee ya Kiafrika inayotumika kwenye Umoja huo na kwamba kutumika kwa lugha ya Kiswahili kutawezesha raia wa nchi za Afrika zaidi ya milioni moja kuweza kufuatilia shughuli za Umoja huo.

Amefafanua kuwa, matumizi ya Lugha ya Kiswahili yatakuza zaidi mtangamano wa Afrika na kuchochea utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara barani Afrika (AfCFTA) kama lugha ya biashara na ya mawasiliano mapana.