
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula amezionya halmashauri nchini kuacha utaratibu wa kubadilisha matumizi ya ardhi bila sababu za msingi.
Dkt Mabula ametoa onyo hilo Jijini Dodoma wakati wa kuhitimisha kikao kazi kilichowaunganisha wakurugenzi wa Halmashauri na wataalamu wa sekta ya ardhi kilichofanyika jijini Dodoma.
" Sasa hivi kila mmoja anaondoa open space anataka kupima viwanja anafuta mashamba anataka kupima viwanja hata kama bado yako katika sura ya kijijini ya kimashamba na anataka kila sehemu kuwe fremu"
Ametolea mfano wa jiji la Dodoma, Dkt Mabula alisema, jiji hilo limeanza kusheheni fremu wakati ni Makao makuu ya nchi na kusema haiwezekani kuwa na miji ya aina hiyo ambayo haipangwi kwenye sura ya makao makuu kwa kujaza fremu na vituo vya mafuta.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi, wapo wataalamu wengi katika sekta ya mipango miji na mabadiliko ya matumizi yasiyo na sababu za msingi hayakubaliki kwa kuwa yanawakosesa hata watoto maeneo ya kucheza sambamba na miji kupumua.
