
Zaidi ya wakazi elfu 30 wa kata mbili za Kalamba na Haubi wilayani Kondoa Mkoani Dodoma wanatarajia kuondokana na adha ya kukosa huduma ya Afya karibu na maeneo yao baada ya serikali kutoa zaidi ya Shilingi Milioni Mia 6 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya kitakachojengwa katika kitongoji cha itongwi.
Naibu waziri wa Fedha na Mipango DKt ASHATU KIJAJI, ametembelea eneo hilo na kushuhudia wananchi wenye ari wakiwa wamejitolea nguvu zao kusafisha eneo ambalo kituo hiko kitajengwa ili kuwaondolea adha ya muda mrefu ya kufuata huduma za afya kondoa mjini umbali wa zaidi ya kilometa 100.
Dkt ASHATU KIJAJI ambaye pia ni mbunge wa jimbo la kondoa vijijini, amepongeza hatua ya baadhi ya wanakijiji cha kalamba kutoa maeneo yao zaidi ya ekari 6 bila kudai fidia ili kuwezesha kuanza kwa ujenzi wa mradi huo unaotarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu ijayo.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa Mkoani Dodoma Dkt IKAJI RASHID amesema kituo hicho cha afya kitakuwa na majengo sita yakiwemo wodi ya wazazi,jengo la upasuaji wa dharula wa akina mama wajawazito,jengo la kuhifadhia maiti na jengo la wagonjwa wa nje.
Kwa upande wao Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya kondoa BI. HIJA BAKARI SURU na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ALHAJI OTHMAN GORA wamewataka wakazi wa kata hizo mbili kujitolea kufanyakazi ili mradi huo ukamilike kwa wakati.