Back to top

UGANDA KUPELEKA WANAJESHI 1000 WA KULINDA AMANI, CONGO

18 November 2022
Share

Msemaji wa Jeshi Uganda, Jenerali Felix Kulaigye, amesema jeshi la nchi hiyo litatuma takriban wanajeshi wake 1000 katika ujumbe wa kulinda amani katika eneo la Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kabla ya mwisho wa mwezi huu.

Vikosi vya Uganda tayari vinajishughulisha kivyake katika eneo hilo, katika misheni ya kivita pamoja na vikosi vya serikali ya Congo dhidi ya Allied Democratic Forces, kundi la waasi wa Uganda lenye kambi nchini humo.

Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya nchi jirani ya Kenya kutuma kundi la pili la wanajeshi wake katika jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC, kushiriki katika ujumbe wa kulinda amani wa kikanda uliokubaliwa mwezi Aprili na nchi saba za Afrika Mashariki ambazo DRC ni sehemu yake, kufuatia kuibuka tena kwa waasi wa M23.

Waasi wa M23 katika wiki za hivi karibuni wameendelea kusonga mbele kuelekea Goma, mji mkuu wa Kivu Kaskazini, huku wakielekea kuweka maeneo zaidi chini ya udhibiti wao.