Back to top

DKT.MABULA AAGIZA VIJIJI VIANDALIWE KUWA MIJI

07 March 2023
Share

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula, ameziagiza Halmashauri zote nchini kuviandaa Vijiji kuwa Miji endelevu ya baadaye na yenye tija kiuchumi na kijamii, ikiwemo kuhimiza upangaji wa vijiji hivyo kwa kuzingatia mwongozo wa upangaji na ujenzi wa nyumba bora vijijini.
.
Dkt.Mabula amesema hayo wakati wa kikao kazi cha kujadili na kuweka mikakati ya kukwamua changamoto za urasimishaji makazi na sekta ya ardhi kwa ujumla,  Mkoani  Geita.

Amesema, moja ya changamoto kubwa inayoikabili nchi kwa sasa  ni kasi kubwa ya ukuaji vitovu vya vijiji  inayoambatana na vijiji hivyo kuendelea kupoteza hadhi  yake ya kuwa vijiji  kwa kusongwa au kumezwa  na tabia za kijamii kwa ukuaji usio endelevu.

Kwa mujibu wa Dkt.Mabula, hali hiyo inatokana na usimamizi na utaratibu duni wa upangaji makazi na ujenzi wa nyumba bora vijijini katika hatua ya awali ya ukuaji.

Ameweka wazi kuwa, upangaji ardhi ya vitovu vya vijiji na miji kwa ujumla ni mwanya mzuri wa kukuza fursa za uwekezaji na kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo kwa wote huku watu wa kipato cha chini wakinufaika kupitia fursa za kibiashara  zitokanazo na uhamiaji na ukaribu kati ya miji midogo na vijiji.

"Tanzania kwa sasa ina vijiji 12,318 kati ya vijiji hivyo zaidi ya vijiji 10,000 sawa na asilimian 80 ya vijiji vyote vimepimwa mipaka yake na kupewa vyeti vya ardhi  vya vijiji ambapo kati ya vijiji hivyo vijiji vyenye mpango ya jumla ya matumizi ya ardhi ni 2, 675 sawa na asilimia 21.7  ya vijiji vyote"Amesema Dkt.Mabula.

Aidha, Waziri Dkt Mabula amesema vitovu vya makazi ya vijiji vingi nchini bado havijaandaliwa mipangokina ya kusimamia na kudhibiti shughuli za ukuaji wake kiuchumi na kijamii na hivyo kupelekea kuwepo changamoto ya ukuaji usio endelevu wa vijiji kama miji tarajiwa ya baadaye.

Alibainisha kuwa, jambo hilo linatokana na mamlaka za upangaji kukosa kipaumbele katika kuzijengea uwezo serikali za vijiji ili kutimiza jukumu hilo  la kuandaa mipango kina ya makazi ili kusimamia ukuaji wake kams miji ys baadaye.

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeandaa Mwongozo wa Upangaji Makazi na Ujenzi wa Nyumba Vijijini mwongozo wenye lengo la kuwasaidia wakijiji kupanga makazi ya vijiji vyao na kujenga nyumba bora na za gharama nafuu kwa njia shirikishi kati ya wataalam wa Mipangomiji, wanavijiji na Wadau mbalimbali.