Back to top

WIZARA YA MALIASILI YAPANIA  KULIIMARISHA JIJI LA DODOMA KIUTALII

03 April 2023
Share

Wizara ya Maliasili na Utalii, kupitia  Idara ya Mambo ya Kale imeanza mkakati maalum wa  kuainisha, kuhifadhi na kuyatangaza maeneo ya kihistoria yanayopatikana katika Jiji la  Dodoma, kwa lengo la kulifanya jiji hilo kuwa na vivutio vya kitalii vya kila aina kama ilivyo katika majiji mengine Duniani

Hatua hiyo inakuja kufuatia kauli aliyoitoa siku chache zilizopita,  Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Mohammed Mchengerwa kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na  vivutio vya utalii vya kila aina, mbali na wanyamapori na kama kila Mtumishi atawajibika ipasavyo idadi ya watalii ifikapo mwaka 2025 itaongezeka maradufu.


Kauli hiyo imemsukuma Mkurugenzi wa Idara ya Mambo Kale, Dkt.Christowaja Ntandu  kutembelea maeneo ya Kihistoria yaliyopo jijini  hapo  kama sehemu ya kufanikisha azma hiyo 

Akizungumza mara baada ya kutembelea Makaburi ya Wahanga wa Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia,  Eneo la mnara wa Uhuru,  Mnara wa Mashujaa wa Tanzania, Nyerere square na Hoteli ya Dodoma, Dkt.Ntandu amesema ziara hiyo ni mkakati maalum wa kushirikiana Wadau wa Utalii katika Jiji hilo kwa lengo la  kuongeza mazao mapya  ya Utalii hususan utalii wa Malikake kwenye maeneo mbalimbali nchini  kuanzia ngazi ya kata mpaka Mkoa

Maeneo mengine aliyotembelea ni pamoja na  eneo Kikuyu ambalo lina asili ya jina la Dodoma, Mti aina ya Mkuyu  uliopo katika eneo la  Chuo Kikuu cha St. John ambao ulitumika kunyongea wahalifu wakati wa Utawala wa Wajerumani


Akizungumzia Hoteli ya Dodoma ambayo licha ya kujengwa  mwaka 1901 lakini bado ipo kwenye hali nzuri, Dkt.Ntandu amesema  sehemu ya jengo hilo ikiwemo vyumba vya kulala wageni na baadhi ya vifaa vikiwemo meza na viti bado vinaendelea kutumika kutokana na  uimara wake.