Back to top

WAFUGAJI WATAKIWA KUJIPANGA NA KUJUA KUWA MIFUGO NI BIASHARA

06 April 2023
Share

Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa kiasi cha shilingi milioni 878. 4, kwa ajili ya kununua madume bora ya Ng'ombe 366 na kuyagawa kwa vikundi vya wafugaji katika Mikoa na Halmashauri za kimkakati, ili kuhakikisha mifugo katika maeneo hayo inaboreshwa na kuongeza tija ya uzalishaji wa nyama.

Hayo yamebainishwa na Waziri Ulega, ambapo amesema Ng'ombe wa asili wana uwezo wa kustahimili magonjwa hata hivyo, pamoja na sifa hizo Ng'ombe hao uzalishaji wao wa nyama na maziwa ni mdogo.

"Ndio maana Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa pesa za kununua haya madume bora ili wafugaji tuweze kuboresha mifugo yetu, tuweze kupata ng'ombe wanaoweza kutoa nyama nyingi"

Mhe.Ulega amesema kufuatia fursa ya masoko ya nyama iliyojitokeza ndani na nje ya nchi, Rais Samia ameona umuhimu wa kuwa na mkakati maalum wa kuboresha mifugo ili izalishe kwa tija.

"Ndugu zangu, nyama ni dili, malisho ni dili, kwa kuthibitisha hilo, katika kipindi cha hivi karibuni nimepokea wageni wengi kutoka nje wakitaka kufanyabiashara ya nyama na nchi yetu"Amefafanua Ulega.

Waziri Mhe.Ulega amebainisha haya wakati wa hafla ya kugawa madume kwa vikundi vya wafugaji iliyofanyika  katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Mkoani Singida.

Ameongeza kuwa madume hayo yatawawezesha wafugaji kuwa na ng'ombe chotara ambao wanauwezo wa kuzalisha wastani wa kilo 150- 200 za nyama ukilinganisha na uzalishaji wa kilo 80-120 kwa Ng'ombe wa asili.  

Naye, Mbunge wa Iramba Mashariki, Francis Mtinga alimshukuru Waziri Ulega kwa kuwezesha wafugaji wa Wilaya ya Mkalama kupata madume Bora 40 huku akimuahidi kuwa watayatumia vizuri madume hayo kuboresha uzalishaji wa mifugo yao.

Halmashauri ambazo zimepata mgao huo ni pamoja na Mkuranga 50, Mvomero 40, Buchosa 46, Chamwino 50, Maswali 50, Chato 50, Msalala 50 na Mkalama 40.