Back to top

WALINDENI WATOTO NA MATUMIZI YA SIMU -DKT.PHILIP MPANGO

09 April 2023
Share

Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, amewasihi wazazi na walezi kuwalinda watoto pamoja na vijana wao dhidi ya matumizi mabaya ya simu pamoja na kufuatilia mienendo yao wakati wote.

Amewaasa wazazi na walezi kulea watoto wao kwa kuzingatia maadili mema ya Kitanzania pamoja na kuwa makini na maudhui ya watoto (Katuni) katika televisheni ili kuwaepusha na kujifunza mambo yasiofaa. 

Makamu wa Rais amesema ni vema kwa wazazi kutambua marafiki wa watoto wao na kuwapa miongozo sahihi wakati wote na kutowaacha kujiongoza wenyewe, Pia amewataka walimu wa shule za msingi, sekondari na hata vyuoni kukemea kwa nguvu uharibifu wa maadili ya kitanzania katika maeneo ya kutolea elimu.

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango akiwa ameongozana na mkewe Mama Mbonimpaye Mpango, ameeleza hayo mbele ya waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska Kiwanja cha Ndege Dodoma katika Ibada ya Jumapili ya Sikukuu ya Pasaka.

Aidha Makamu wa Rais amewaasa waumini na Watanzania kwa ujumla kuongeza jitihada katika ulinzi na uhifadhi wa mazingira, kwa kupanda miti katika kila kaya pamoja na usafi katika maeneo yao, Ni vema wazazi kutoa mafunzo kwa watoto wao namna ya kupanda miti na kuisimamia.