
Serikali imesema itatenga shilingi bilioni 27.9, katika Mwaka wa Fedha wa 2023/24, kwa ajili ya ukarabati wa hospitali kongwe thelathini na moja.
Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mhe.Festo Dugange amesema hayo bungeni wakati akijibu Swali la Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki Mhe.John Pallangyo, aliyetaka kujua mpango wa serikali kukarabati miundombinu ya Hospitali ya Wilaya ya Arumeru.
Mhe.Dugange amesema katika mwaka wa Fedha wa 2022/23 serikali ilitenga shilingi bilioni kumi na saba nukta moja kwa ajili ya ukarabati wa hospitali kumi na tisa ambapo hadi kufikia Februari, 2023, shilingi bilioni 12.95 zimetolewa kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya hospitali kongwe kumi na nne.
Amesema katika mpango huo hospitali ya Halmashauri ya Meru, imetengewa Shilingi milioni mia tisa.
Katika hatua nyingine amesema katika mwaka wa fedha 2022/23, serikali ilitenga shilingi bilioni thelathini na tano nukta moja kwa ajili ya ununuzi wa magari mia tatu kumi na sita ya kubebea wagonjwa.
Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Mufindi Kusini Mhe.David Mwakiposa, aliyetaka kujua mkakati wa serikali katika kupeleka magari ya kubebea wagonjwa katika vituo vya afya vya Mtwango na Mgololo.
Amesema taratibu za manunuzi zinaendelea na magari hayo yatagawiwa kwenye halmashauri zote mia moja themanini na nne ambapo kila Halmashauri itapewa magari mawili.
