
Serikali imepiga marufuku operesheni zote zinazofanyika kwa kuviziana baina ya mamlaka za hifadhi na wananchi, wanaoishi katika maeneo yanayopakana na hifadhi na imehimiza ushirikishwaji wa wananchi katika hatua zote ikiwa ni pamoja na kupewa taarifa.
Agizo hilo limetolewa na Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa bungeni Dodoma, wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo, wakati akitoa taarifa ya serikali juu ya namna inavyoshughulikia jambo hilo na kuzitaka mamlaka husika zichukue hatua zaidi kudhibiti migogoro katika maeneo hayo.
Mhe.Majaliwa amewataka wahifadhi wahakikishe wanawazuia mapema wananchi kuanzisha shughuli za kilimo, ufugaji na makazi ndani ya hifadhi, ili kuepuka uhitaji wa kuondoa shughuli ambazo zineshaanzishwa kama vile kuvunja makazi, kufyeka mazao au kukamata mifugo.
Aidha, amelielekeza Jeshi la Polisi kuchunguza kwa umakini matukio yote yaliyotolewa taarifa na waheshimiwa wabunge na wananchi kuhusu kuteswa, kuumizwa na kuuawa kwa baadhi ya wananchi waliotuhumiwa kuingia ndani ya hifadhi, ili watakaobainika kukiuka sheria wachukuliwe hatua stahiki.
