
Wananchi wa Vijiji viwili vya Mwamanimba na Mwamatiga, vilivyopo Wilayani Meatu mkoani Simuyu, vyenye wakazi zaidi ya elfu mbili wameingia hofu ya kukumbwa na baa la njaa, baada ya mazao yao ya nafaka zaidi ya hekari mia moja kuungua na jua lililosababishwa na hali ya ukame, uliotokea miezi miwili iliyopita huku mengine yakishambuliwa na wadudu waharibifu aina ya viwavi jeshi.
Kutokana na hali hiyo, wananchi wa Vijiji hivyo, wameiomba serikali kupeleka timu ya wataalam, ili kukabiliana na wadudu hao ikiwa ni pamoja na kuwapelekea chakula kitakachouzwa bei rafiki ili waweze kukabiliana na hali hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa divisheni ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Bwana Thomas Masanja, anakiri baadhi ya maeneo kuathirika na tayari hatua za awali zimekwisha chukuliwa ikiwa ni pamoja na kupambana na wadudu hao huku akiwaomba wananchi wa maeneo hayo kutunza chakula kitakachopatikana.
