
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kusini imechoma kilo 600 za mifuko ya plastiki na tani tano ya kemikali iliyokwisha muda wake, huku ikisisitiza wamiliki wa viwanda na jamii kwa ujumla kutii sheria ya usimamizi wa mazingira ili kulinda afya ya jamii na mimea.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa baraza hilo Kanda ya Kusini, Mhandisi Boniphace Guni katika wiki ya mazingira iliyokwenda sambamba na zoezi la uchomaji taka lililofanyika katika kiwanda cha Saruji cha Dangote.
Katika kuadhimisha wiki ya mazingira kanda ya kusini imefanikiwa kuchoma mifuko ya plasitiki miasita yenye thamani ya shilingi milioni nne na kuwasihi wafanyabiashara kuacha kutumia mifuko iliyokatazwa na badala yake kutumia mifuko mbadala iiliyopitishwa na NEMC.
Amesema NEMC Kanda ya Kusini haitasita kuwachukulia hatua wale wote watakao kaidi sheria ikiwa ni pamoja na kutozwa faini huku akisisitiza wamiliki wa viwanda kufuata sheria pale wanapoitaji kuchoma taka zenye kemikali ili kuepuka kuharibu mazingira.
Kwa upande wake Afisa wa Mazingira kutoka kiwanda cha Saruji cha Dangote, Mohammed Bakari amesema kiwanda kiko tayari kupokea taka kutoka kwa wadau na kuwataka kuwa na kibali maalumu kutoka NEMC.
