Back to top

NYAMA YA TANZANIA KUANZA KUUZWA NCHINI MISRI

12 June 2023
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amekutana Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Taifa ya Huduma za Miradi (NSPO) Meja Jenerali Hossam Nigeda wa Misri aliyeongozana na ujumbe wake.

Ulega amekutana na ujumbe huo kujadiliana namna ya kuanza kufungua soko la nyama ya Tanzania nchini Misri.

Katika mazungumzo yao, Meja Generali Nigeda amesema lengo lao ni kuendelea kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo mbili kwa kufungua soko la nyama ya Tanzania nchini Misri.

Ameongeza kuwa wamejipanga kuanzisha machinjio ya kisasa Tanzania ambayo itawawezesha kusafirisha tani 600 ya nyama kila Mwezi, pia kusafirisha wanyama hai wakiwemo ng'ombe, kondoo na mbuzi 10,000 kila Mwezi.

Alifafanua kuwa kwa siku za hivi karibuni wapo katika mipango ya kusafirisha tani 100 za nyama kabla ya sikukuu ya Eid Al Hajj ili kuanza kutangaza soko la nyama ya Tanzania nchini humo.

Misri ni miongoni mwa nchi zenye Idadi kubwa ya watu barani Afrika ambapo Idadi ya watu wake hawapungui Milioni 120 hivyo itakuwa fursa nzuri ya kibiashara kwa Tanzania hususan biashara ya nyama.

Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amemuhakikishia Meja Jenerali Nigeda kuwa Tanzania ipo tayari na watawapa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha biashara hiyo iweze kuanza haraka iwezekanavyo.

Wajumbe wengine waliombatana na Meja Jenerali Nigeda ni Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Taifa ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji, Islam Attia Abdel Hamid, Mwenyekiti wa Huduma za Mifugo, Misri, Meja Jenerali, Dkt. Ihab Saber Youssef na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Masr Trading, Dkt. Hatem Ahmed.

Ziara hiyo ni miongoni mwa jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kufungua milango ya kibiashara nje ya nchi.