Back to top

“KIKAO CHA BARAZA KITOKE NA MAAMUZI YENYE TIJA” MHAGAMA.

12 March 2025
Share

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama alitaka Baraza la watumishi wa Wizara ya Afya na Taasisi zake mijadala yao ilenge kuleta tija na ufanisi ili kuendelea kuinua sekta ya afya nchini. 

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Machi 12, 2025 wakati akifungua kikao cha Baraza la wafanyakazi la Wizara ya Afya kinachofanyika mkoani Mwanza, chenye lengo la kuwawezesha watumishi kushiriki kikamilifu katika uongozi wa pamoja mahali pa kazi na kuimarisha mahusiano kati ya wafanyakazi na waajiri katika ngazi zote za Wizara.

"Natumaini kuwa maamuzi yatakayofikiwa hapa kwenye kikao chetu  muhimu, yatakuwa na mchango mkubwa katika kuinua Sekta ya Afya kwa maslahi mapana ya Wizara na Taifa kwa ujumla, kwa msingi huo, nawasihi tushiriki mijadala yenye tija, tukijadili kwa kina na kwa mtazamo wa kujenga," amesema Waziri Mhagama.

Amesema, kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya Mwaka 2002 pamoja na kanuni zake za mwaka 2005, Baraza hilo ni chombo muhimu cha majadiliano na maamuzi yanayolenga kuimarisha mahusiano kati ya wafanyakazi na waajiri katika ngazi zote za Wizara. 

Aidha, Waziri Mhagama amesema katika utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2024/25, Wizara  imefanikisha utekelezaji wa ufadhili wa masomo kupitia 'Samia Health Specialized program' ambao umewezesha ufadhili wa masomo kwa watumishi wa Sekta ya Afya 544 na kufanya jumla ya watumishi 1,455 kupata ufadhili wa kusomea fani za ubingwa na ubingwa bobezi. 

"Tumeiimarisha hali ya upatikanaji wa bidhaa za Afya katika vituo vya kutolea huduma za afya kufikia wastani wa asilimia 83 ambapo kiasi cha Shilingi Bilioni 103.3 kimetumika, kusimika mashine za Digital X-ray katika baadhi ya hospitali za rufaa za mikoa, usimikaji wa PET CT Scan 45, MRI 13, Digital X-ray 491 pamoja na Ultra Sound 512 katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini," amesema Waziri Mhagama.

Baraza hilo la wafanyakazi litajadili na kufanya maamuzi kuhusu ajenda kuu tano (5) muhimu ikiwemo kujadili na kupitia utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2024/25, mapendekezo ya Bajeti ya mwaka 2025/26, kupata mrejesho kuhusu rasimu ya miundo ya maendeleo ya utumishi ya kada za Afya.

Vilevile katika kikao hicho watajadili namna ya kupata taarifa ya mkakati wa utoaji wa huduma na utendaji kazi wa Wizara katika kuboresha huduma za Afya nchini, kupata taarifa za utekelezaji na ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi pamoja na masuala yanayohusu maslahi ya watumishi.

Awali Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe alisema kikao cha Baraza la Wafanyakazi lipo kwa mujibu wa sheria ili kudumisha mahusiano mema kazini baina ya waajiriwa na muajiri hivyo akawasihi wajumbe kushiriki na kufuatilia mada zote zitakazoletwa mbele yao.