Back to top

BARABARA YA BOMANG'OMBE YAKAMILIKA KWA LAMI

03 March 2024
Share

Serikali kupitia Wakala wa Barabara(TANRADS), kwa kipindi cha miaka mitatu,  imesema imefanikiwa kukamilisha na kutekeleza miradi mbalimbali ya barabara Mkoani Kilimanjaro ikiwemo ukarabati na ujenzi wa kiwango cha lami, barabara ya Bomang’ombe – Sanyajuu – Kamwanga yenye urefu wa kilomita 96.03, sehemu ya Sanyajuu – Elerai km 30.62.
.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kilimanjaro Mha. Motta Kyando amesema utekelezaji wa ujenzi wa kiwango cha lami unaendelea kwenye barabara mbalimbali ikiwemo barabara ya Same – Kisiwani – Ndungu – Mkomazi km 98, Holili (Rotima) Tarakea – Nayemi km 52.8 na barabara ya Bomang’ombe – Sanyajuu km 24.91.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi Motta Kyando


Amesema katika barabara ya Holili – Tarakea Nayemi katika mwaka wa fedha 2024, Serikali imejipanga kuendelea na ujenzi wa sehemu ya km 10 ambapo maandalizi ya manunuzi yanaendelea, Elerai – Kamwanga, Serikali imekwisha fanya manunuzi na kumpata Mkandarasi atakayetekeleza kazi hiyo, maandalizi ya ujenzi wa awamu ya pili Same – Maore km 56.8 na awamu ya tatu Ndungu- Mkomazi km 36 yapo katika hatua za mwisho za manunuzi.
.
Ameeleza katika barabara ya Arusha – Moshi – Holili; Sehemu ya Moshi – Himo – Holili maandalizi ya kumpata Mhandisi Mshauri wa kufanya mapitio ya usanifu wa kina yameanza katika Ofisi za Wakala ya barabara ili kubaini upanuzi wa barabara katika eneo la Moshi Mjini na ukubwa wa daraja jipya la Kikafu.
.
Amesema pia Ofisi ya TANROADS Mkoa wa Kilimanjaro inaendelea na upembuzi wa yakinifu na usanifu wa kina wa miradi ya barabara ya Kisangara – Nyumba ya Mungu km 17.5 na barabara ya Same – Himo – Marangu km 99.7.
.
Mha. Motta Kyando ameeleza kuwa miradi hiyo  inatekelezwa na Wakandarasi Wazawa na imesaidia kuongeza ukuaji wa Uchumi katika kandarasi zao na kuwajengea uwezo wa kutekekeleza miradi ya maendeleo na imewasaidia Wananchi wa maeneo husika kunufaika na ajira zilizowasaidia katika kuwainua kiuchumi pamoja na huduma kwa usafirishaji wa urahisi kwenye shughuli zao za kila siku.