
Mgombea urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema wananchi wa Wilaya ya Mwanga watanufaika na miradi mikubwa ya miundombinu na maji, hatua itakayochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Dkt. Samia amesema barabara kuu zenye urefu wa zaidi ya kilomita 100 zitajengwa kwa kiwango cha lami, ikiwemo Kikweni – Vuchama, Kisangara – Shighatini, Usangi – Kwakihindi, Jipe – Kambi ya Simba, Mgagao – Karamba – Toloha, Kilomeni – Sofe – Mringeni, Mriti – Kambi ya Simba na Mlembea – Kivanda – Tangwa.
Aidha, amebainisha kuwa serikali itatekeleza miradi ya maji katika maeneo ya Masumbeni–Kadengere, Ubembe–Kitiriko, Nyumba ya Mungu, Mwai, Mangio, Mwaniko, Lambo, Kileo–Kivulini na Kimbale, sambamba na ujenzi wa tanki la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita 50,000 kwa Hifadhi ya Mkomazi.
Kwa upande wa elimu, amesema vyumba vya madarasa 315 vitajengwa katika shule za msingi na vyumba 85 kwenye shule za sekondari, hatua itakayopunguza msongamano wa wanafunzi.