
Airtel Tanzania, kupitia kitengo cha huduma kwa biashara, imesogeza suluhisho za mawasiliano na huduma za kidijitali kwa wafanyabiashara katika Maonesho ya Kitaifa ya Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), yanayofanyika katika Viwanja vya Magufuli, Manispaa ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga, kuanzia Oktoba 21 hadi 30, 2026.
Maonesho hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, yanashirikisha zaidi ya wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo 600 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.


Akizungumza wakati wa ufunguzi, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, alisema Serikali inaendelea kupanua upatikanaji wa mikopo kwa wajasiriamali ili kukuza biashara, kuongeza uzalishaji na kutengeneza ajira, huku akihimiza taasisi za fedha kushirikiana na SIDO kubuni huduma zinazokidhi mahitaji ya wafanyabiashara.
Kapinga pia aliitaka SIDO kuelekeza mikopo zaidi katika shughuli za uzalishaji na uongezaji thamani wa bidhaa ili kuimarisha viwanda vya ndani na kuongeza fursa za ajira. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Airtel Business, Joseph Vipond, alisema ushiriki wa kampuni hiyo katika maonesho hayo ni sehemu ya dhamira yake ya kuwawezesha wafanyabiashara kupata suluhisho za kidijitali nafuu na za kuaminika zinazosaidia kuboresha ufanisi na kukuza biashara zao.
