
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto imeweka mkakati wa kusogeza karibu huduma za tiba asili kwa jamii ambazo sasa dawa hizo asilia zinawekewa mikakati ya kupatikana hadi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na maduka ya kuuza dawa za binadamu.
.
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi mara baada ya kufanya kikao na wazalishaji wa dawa hizo asilia nchini ambao dawa zao zimethibitishwa Usalama na Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na Msajili wa Tiba Asili nchini na kukidhi vigezo vya kutumika kwa binadamu.

“Sisi watendaji tumeona ni muhimu kukutana ili tuweze kuweka mikakati ya kuhakikisha hizi dawa za asili zinawafikia wananchi kwa urahisi zaidi”amesema Prof. Makubi.
.
Amesema kuwa tunasumbuliwa na magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza hivyo ni lazima tutumie silaha (dawa asilia na za kisasa) zote ambazo ni salama na zinaweza kusaidia wananchi kwa afya.
.
Aidha Prof. Makubi amewataka wasomi na wataalam wa afya kwa ujumla kubadili mtazamo wao juu ya tiba asili kwa kuwa zimekuwa na mchango mkubwa wa kutibu magonjwa mbalimbali ya binadamu na kuwaasa wataalam kutokuwa kikwazo kwa wananchi kutumia tiba asili.
.
“Kama dawa sisi tumeshaihakiki na tukaikubali kwamba hii dawa ni salama, basi pasiwepo na kinyongo au ugumu wowote wa sisi watumishi wa afya kuruhusu mwananchi kutibiwa kwa dawa hiyo ”Amesisitiza Prof. Makubi.