Back to top

Epa, Kiwira, ununuzi wa rada ya serikali vyamtesa Mkapa.

12 November 2019
Share

Rais wa awamu ya tatu, Mhe.Benjamini William Mkapa amesema katika kipindi cha utawala wake yapo mambo yaliyotokea ambayo mpaka sasa  yamekuwa yakimsikitisha.

Mambo hayo ni pamoja na la EPA, uuzwaji wa Mgodi wa Kiwira, ubinafshaji wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kwa Netgroup Solution, ununuzi wa Rada ya Serikali ambao uligubikwa na udanganyifu mkubwa na baadhi ya watu kumwita yeye ni dikiteta kutokana na kusimamia   mambo aliyoyaamini.

Hayo yamesemwa na Prof.Rwekaza Mukandala wakati akitoa uchambuzi wa kitabu kilichoandikwa na  Mhe.Mkapa kinachoitwa My Life, My Purpose, ambacho kimezinduliwa na Rais wa awamu ya tano Dkt.John  Magufuli Jijjini Dar Es Salaam.

Mhe.Mkapa pia amesema ameona ni vyema kuandika kitabu hicho ili kuweka kumbukumbu sahihi ya mambo mbalimbali, ambayo amefanya wakati  wa uongozi wake na maisha kwa ujumla ili kutoa somo kwa wengine.

Kabla ya kuzindua kitabu hicho Rais John Magufuli amempongeza Mhe.Mkapa kwa kuandika kitabu hicho na kumtaja kama mtu imara na  asiyekubali kuyumbishwa na kuwataka Watanzania waige mfano huo.

Kitabu hicho kimefadhiliwa na Serikali ya Finland chini ya uratibu wa Taasisi ya Uongozi ambapo Afisa Mtendaji wake Mkuu, Prof.Joseph Semboja amesema haikuwa rahisi kuandika kitabu hicho.

Sherehe hizo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali ambapo uzinduzi wa kitabu hicho umekwenda pamojana maadhimisho ya miaka 81 tangu kuzaliwa kwa Mhe.Mkapa.