Back to top

IDADI YA WAGONJWA WA MOYO YAONGEZEKA

29 September 2023
Share

Wizara ya Afya imesema kulingana na takwimu za Mfumo wa Taarifa za Uendeshaji wa Huduma za Afya (MTUHA), zinaonyesha kuwa kuna ongezeko la 9.4% ya magonjwa ya moyo na shinikizo la juu la damu, ambapo hadi mwaka 2022 wagonjwa Mil. 3.4 wameongezeka kutoka wagonjwa Mil. 2.5 mwaka 2017.


.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Mhe.Ummy Mwalimu,kwenye Maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Dar Group iliyopo Temeke jijini Dar es Salaam.


Aidha Waziri Ummy amesema, Magonjwa ya Moyo na ugonjwa wa Kiharusi yanaweza kuzuilika kwa mtu mmoja mmoja na jamii yetu kwa kuweza kuchukuwa hatua za haraka. 

“Kwa mujibu wa maelezo ya wataalam sababu zinazopelekea kuongezeka kwa magonjwa Yasiyoambukiza ikiwemo Magonjwa ya Kiharusi ni pamoja na kutozingatia ulaji unaofaa ambapo kwa nchi yetu inaonesha asilimia 3 tu ya watu wazima wanatumia kiasi cha wastani wa kutosha cha matunda na mbogamboga”. Amesema Waziri Ummy

Pia Waziri Ummy amesema kupunguza matumizi yaliyokithiri ya chumvi, sukari na mafuta ya kupikia kwa kuzingatia ushauri wa muhimu unaotolewa na madaktari  kwa kufanya hivi kutaweza kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo tatizo la Moyo.