
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha ujenzi wa Mfumo wa Usimamizi wa Kodi za Ndani ujulikanao kama IDRAS, ambao unalenga kuleta mapinduzi makubwa katika ukusanyaji na usimamizi wa kodi nchini.
Hayo yameelezwa leo Mkoani Morogoro na Meneja wa Mradi wa IDRAS, Bw.Frank Mwaselela, wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo Vinara 105 wa Usimamizi wa Mabadiliko kutoka Tanzania Bara na Visiwani.
Bw. Mwaselela amesema mfumo huo utarahisisha kazi ya ukusanyaji wa kodi kwa kuiunganisha taratibu zote za kodi za ndani kwenye jukwaa moja la kidijitali.
“IDRAS ni mfumo ambao utarahisisha upatikanaji wa taarifa, uwasilishaji wa taarifa za kodi, na ufuatiliaji wa malipo. Unalenga kuleta urahisi wa matumizi kwa watumiaji wa ndani wa TRA, hasa maofisa wa ukusanyaji,” amesema Bw. Mwaselela.
Ameeleza kuwa katika hatua za ujenzi wa mfumo huo, TRA imeshirikiana kwa karibu na wadau wa ndani na nje ya taasisi ili kuhakikisha kuwa mfumo huo unajengwa kulingana na mahitaji halisi ya watumiaji katika ulimwengu wa kisasa wa Usimamizi wa kodi, sheria na taratibu za kodi.
“Tumeweza kuyapitia mahitaji mbalimbali ya wadau ili kuhakikisha tunajenga mfumo unaokidhi matakwa ya sasa ya kiteknolojia na kiutendaji. Kwa sasa tupo kwenye hatua ya mwisho ya ujenzi,” aliongeza”, Bw. Mwaselela .
Kwa mujibu wa Mwaselela, hatua muhimu kabla ya mfumo kuanza kutumika ni kuwaandaa watumiaji wa ndani na nje kwa kuwajengea uwezo juu ya namna ya kutumia mfumo huo.
“Kwa sasa tupo kwenye tukio maalum ambalo linawaleta pamoja watumiaji wa ndani kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani, zaidi ya 105. Lengo ni kuwapa mafunzo na kuwawezesha kuwa mabalozi wa mfumo huu katika maeneo yao ya kazi,” amesema.
Vile vile amesema kuwa mfumo huo mpya utachukua nafasi ya utaratibu wa zamani wa usimamizi wa kodi uliokuwa ukifanyika kwa njia zisizo za kielektroniki. Kwa sasa, taratibu zote zitaendeshwa kwa njia ya kidijitali, jambo ambalo litaongeza uwazi, ufanisi na uwajibikaji.
“Mabadiliko haya ni makubwa na yanahitaji maandalizi ya kina kwa watumiaji. Tumeanza na kuwanoa mabalozi wa ndani, na baadaye tutafikia makundi mengine wakiwemo watumiaji wa nje ya taasisi,” ameeleza Bw. Mwaselela.