Back to top

KLINIKI MAHSUSI YA AFYA YA AKILI YAFAUNGULIWA MNH

04 September 2025
Share

Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kuzuia Kujiua Duniani tarehe 10 Septemba, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Delilah Kimambo, amezindua kliniki mahsusi ya afya ya akili kwa ajili ya wafanyakazi wa hospitali hiyo  inayolenga kutoa huduma za ushauri, uchunguzi na tiba ya changamoto za kisaikolojia, ikiwamo mfadhaiko na msongo wa mawazo unaoweza kuchochea tabia za kujiua.

Akizungumza na wafanyakazi wa MNH leo Jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa afua mbalimbali zitakazofanywa na hospitali kuelekea siku hiyo, Dkt. Kimambo ameeleza kuwa hatua hii ni sehemu ya mkakati wa kitaifa na kimataifa wa kudhibiti ongezeko la matukio ya kujiua na majaribio yake.

 “Tumeona ni muhimu kuwapa kipaumbele wafanyakazi wetu kwani wao ndio nguzo ya huduma za afya. Kliniki hii itasaidia kuondoa unyanyapaa, kutoa msaada wa haraka, na kuimarisha afya ya akili ili kuhakikisha kila mmoja anahisi kuthaminiwa na kuungwa mkono.” amesema Dkt. Kimambo

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), za mwezi Machi mwaka 2025, kulikuwa na visa vya kujiua zaidi ya  720,000 ambapo wanaume wanaongoza mara mbili  zaidi ya wanawake katika matukio hayo.

Aidha, vifo vitokanavyo na kujiua vinashika nafasi ya tatu duniani kwa vijana wenye umri wa miaka 15–29 ambapo zaidi ya asilimia 73 ya vifo hivyo hutokea nchi zenye kipato cha chini na cha kati.