Back to top

MNYETI ASHUSHA NEEMA YA RAIS SAMIA KWA WAVUVI MBEYA, NJOMBE, RUVUMA.

16 November 2023
Share

Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti amekabidhi boti 4 za Uvuvi za mkopo usio na riba zenye thamani ya shilingi milioni 229.9 kwa wavuvi wa mikoa ya Mbeya, Njombe na Ruvuma. 

Mnyeti amewataka wavuvi hao kuhakikisha wanarejesha mikopo ya boti hizo kwa wakati uliopangwa, ili kuiwezesha Serikali kununua boti nyingine za kuwakopesha wavuvi wengine, ambapo ameongeza kuwa Serikali italazimika kuchukua boti hizo kwa wale wote watakaoshindwa kurejesha mikopo hiyo na kuwapa watu wengine.

Mnyeti amebainisha hayo Katika hafla iliyofanyika kwenye bandari ndogo ya Kiwira iliyopo Wilaya ya Kyela mkoani mbeya, iliyohudhuriwa na Wakuu wa mikoa ya Mbeya na Rukwa, Mhe. Mnyeti amesema kuwa boti hizo zenye vifaa vya kisasa zimetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kubadili maisha ya wavuvi wa Ziwa Nyasa na kuwaondoa kwenye uvuvi wa kutumia zana duni waliokuwa wakiufanya hapo awali.

Kwa upande wake mwakilishi wa mikoa iliyonufaika na mkopo huo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Kanali Laban Thomas mbali na kumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia kwa kutoa boti hizo amewataka. wavuvi waliokabidhiwa kuhakikisha wanazitumia kubadili mfumo mzima wa utekelezaji wa shughuli zao za Uvuvi ili ziweze kuwa na tija na kuongeza pato lao na lile la Taifa.

Naye mmoja wa wanufaika wa boti hizo kutoka Wilaya Kyela  mkoani Njombe Bw. Gabriel Kipiga amesema kuwa mkopo wa boti hizo utakuwa ni mwarobaini wa kuwaondoa kwenye Uvuvi wa kubahatisha na kuhamia kwenye Uvuvi wa kisayansi utakaochagizwa na matumizi ya vifaa vya kisasa vya kutambua maeneo yenye samaki wengi (fish finder).

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa zoezi hilo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mkurugenzi wa Utafiti,Mafunzo na Ugani kwa upande wa sekta ya Uvuvi Prof. Mohammed sheikh amesema kuwa thamani ya mradi wote kwa ujumla ni shilingi Bilioni 11.5 ambapo boti hizo zina injini za kupachika, kifaa maalum cha kuonesha mahali samaki walipo (fish finder), koti maalum la uokoji majini, nyavu za kuvulia na kifaa cha kuongozea uelekeo wa boti (GPS).