Back to top

Naibu Waziri TAMISEMI anusurika kifo katika ajali Chalinze.

07 April 2018
Share

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - TAMISEMI - Mheshimiwa JOSEPH KAKUNDA amenusurika katika ajali, baada ya gari aliyokuwa akisafiria kuacha njia na kupinduka mara tatu, katika eneo la Mboga Chalinze, barabara kuu ya Chalinze-Segera.

Akizungumza katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro aliko pelekwa baada ya ajali, amesema alikuwa akitokea Mererani Mkoani Manyara kushuhudia uzinduzi wa ukuta uliofanywa na Rais.Dakta JOHN MAGUFULI kwenda Mjini Morogoro kufunga mafunzo kwa walimu wa MEMKWA yanayofanyika katika Chuo cha Ualimu Morogoro.

Amesema baada ya dereva wake kufika eneo la Mboga, dereva wake aliona mtu akikatiza mbele yake na kujaribu kumkwepa, lakini gari ikapinduka mara tatu na kuharibika vibaya, ingawa yeye, dereva wake na katibu wake waliokuwa ndani ya gari hiyo wote walitoka salama.

Naibu waziri huyo aliyepumzishwa awali katika wadi maalum ya daraja la kwanza katika hospitali hiyo ya rufaa ya Mkoa wa Morogoro, baada ya kupatiwa vipimo na kuonekana yuko salama, akiambatana na mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dakta. KEBWE STEPHEN KEBWE na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Bi. REGINA CHONJO, ametumia fursa hiyo kuwajulia hali wagonjwa waliolazwa wadini na kuzungumza na wafanyakazi wa hospitali hiyo.