Back to top

POLISI KUNUNUA MBWA WA KUDHOOFISHA WAHALIFU

10 February 2026
Share

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura, amesema Jeshi la Polisi litaendelea kuweka jitihada za kununua mbwa wapya wa kisasa na wenye uwezo, ili kuboresha muonekano wa mbwa wa Polisi mwenye umbo lenye kumdhoofisha mhalifu.

IGP Wambura, ameyasema hayo wakati wa Ufunguzi wa Kikao Kazi cha Wakuu wa Kikosi cha Mbwa na farasi wa Mikoa na Wataalam Waongoza Mbwa na Farasi kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam, huku akiweka msisitizo kwenye eneo la utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuwatumia Wanyama kazi, katika kudhibiti uhalifu kwenye maeneo yao.

Akizungumza na Watendaji hao IGP Wambura, amebainisha kuwa Kikosi hicho kina umuhimu mkubwa kiusalama, kwa kuwa doria za mipakani na maeneo mengine muhimu hulazimika kutumia mbwa na farasi, kwani ni rahisi kupenya kwenye maeneo
ambayo gari haliwezi kupita kwa urahisi.

Amesema, Jeshi la Polisi lina Mbwa na Farasi wanaofanya kazi katika bandari, viwanja vya ndege na mipakani kwa lengo la kuzuia biashara za magendo na usafirishaji haramu wa silaha pamoja na dawa za kulevya, hivyo amewataka kuendelea kuweka nguvu ya kutosha kuhakikisha kuwa, muda wote mipaka yetu inakuwa salama kwa kushirikiana na askari kutoka vikosi vingine ili kudhibiti uhalifu.