Back to top

RC Wangabo aonya wanafunzi kuhusu mimba mashuleni.

25 April 2018
Share

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewatahatharisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kuwa makini na kushiriki katika tendo la ndoa katika umri mdogo kwani kufanya hivyo wanajiweka katika hatari ya kupata saratani ya mlango wa kizazi.

Amesema kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia kupata saratani ya mlango wa kizazi ni pamoja na kushiriki katika tendo la ndoa na wapenzi wengi, kuzaa watoto wengi, ndoa za mitala pamoja na uvutaji wa sigara.

“Tangu mwaka 2015 hadi 2017 kumekuwa na mimba 325 huku shule za msingi kukiwa na mimba zaidi ya 20, huu ni ushahidi kuwa wanafunzi mnashiriki katika vitendo hivi katika umri mdogo, tukijua wazi kuwa mwananfunzi wa shule ya msingi anamaliza shule akiwa na umri wa miaka 13 au 14 na wengi katika shule za sekondari, hili tendo linachangia upatikanaji wa saratani,” Alisisitiza.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akimhoji mwanafunzi aliyepata chanjo Gift Ndenje wakati wa uzinduzi wa chanjo hiyo uliofanyika katika shule ya sekondari Mazwi 24/4/2018. 

Ameyasema hayo alipokuwa akizindua chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi iliyofanyika katika viwanja vya shule ya sekondari Mazwi ikishirikisha wanafunzi kutoka katika shule mbalimbali za msingi na sekondari zilizopo katika manispaa ya Sumbawanga.

Kwa upande wake mwakili wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Boniface Mokelemo ameusifu Mkoa wa Rukwa kwa kufanya vizuri katika mazoezi ya chanjo nyingine zinazoendelea nchini hivyo kuwa na Imani kuwa chanjo hii itafanya vizuri zaidi na kuwasihi wananchi kuhimizana kupata chanjo hiyo.

Katika kuliweka sawa hilo mganga mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu ameongeza kuwa mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa mikoa ilifanya vizuri kwa kuwafikia watoto wengi na kina mama wengi kupata chanjo kama surau, polio, pneumonia, na homa ya uti wa mgongo hali iliyopelekea kupungua kwa magonjwa mengi kwa watoto chini ya umri wa mwaka mmoja.

Kwa upande wao wanafunzi waliopata chanjo hiyo wamewaasa wanafunzi wenzao kutoogopa kushiriki kupata chanjo hiyo kwani itawasaidia kuwakinga na ugonjwa huo hatari wa saratani ya mlango wa kizazi na kuiomba serikali iweze kuwafikia wasichana wengi ili kuokoa maisha yao.