Back to top

SAMIA AAHIDI KUINUA MAENDELEO MANYONI KUPITIA ELIMU, MAJI, NISHATI

09 September 2025
Share

Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea na kampeni zake za Uchaguzi Mkuu 2025 kwa kufanya mkutano mkubwa wa hadhara Wilayani Manyoni, Mkoa wa Singida, ambako ametaja utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo na kuahidi kuimaliza ndani ya awamu yake ijayo.

Dkt. Samia amesema Serikali ya CCM imeweka kipaumbele kwenye sekta ya elimu kwa kuhakikisha ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Manyoni unakamilika, ili vijana wapate ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kushiriki katika uchumi wa viwanda.

Katika sekta ya maji, amewahakikishia wananchi kuwa mradi wa maji wa miji 28 utakamilishwa na kutoa suluhisho la kudumu kwa changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Akigusia sekta ya miundombinu, Dkt. Samia ametaja ahadi za CCM 2025 kuwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa barabara na daraja, zikiwemo barabara zinazounganisha Manyoni East – Sanza – Chali na Igongo – Dodoma Mjini, ambazo zitafungua fursa za biashara na kuongeza mzunguko wa uchumi kwa wananchi wa Manyoni na mikoa jirani.

Vilevile, ameeleza kuwa serikali itasimamia utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu ya jua katika Kihamba – Manyoni, mradi utakaoongeza upatikanaji wa nishati safi, nafuu na endelevu.

"CCM tumethubutu, tumetekeleza na tunaendelea kutenda. Miradi hii yote ni sehemu ya ahadi tulizoziweka Manyoni na Singida kwa ujumla, na nina hakika kupitia mshikamano wetu tutaipeleka Tanzania mbele zaidi"Ameema Dkt. Samia.