
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, kadri uchumi unavyokua kwa kasi mahitaji ya nishati hasa Gesi Asilia yanaongezeka hivyo Serikali inaendelea na jitihada za kuendeleza miradi ya mkondo wa juu wa petroli kwa lengo la kugundua na kuendeleza vyanzo vipya vya rasilimali za Mafuta na Gesi Asilia.
“Nampongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuendeleza mkondo wa juu wa petroli ambapo chini ya uongozi wake uzalishaji wa gesi umeimarika katika vitalu vya Songosongo na MnaziBay ambavyo ni muhimu katika uchumi wa gesi.”Amesema Dkt.Biteko
Dkt. Biteko ametaja baadhi ya mafanikio katika Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia nchini kuwa ni pamoja na uendelezaji wa gesi asilia iliyogunduliwa katika eneo la Ntorya kitalu cha Ruvuma kwa kutoa leseni uendelezaji wake kwa kampuni ya ARA Petroleum na kuongezeka kwa ushiriki wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kitalu cha Mnazibay kutoka asilimia 20 hadi 40.
Naye Waziri wa Nishati wa Uganda, Mhe. Ruth Nankwabira Seitamo, ameeleza kuhusu umuhimu wa fedha zinazopatikana katika Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia kunufaisha Sekta nyingine huku akitolea mfano kuwa nchini Uganda wameanzisha Mfuko wa Petroli ambao unahudumia sekta nyingine ikiwemo barabara, elimu, afya lengo likiwa ni kuhakikisha kila mtu anafaidika na sekta husika.
Amesema sekta ya Mafuta na Gesi ni muhimu katika kuelekea kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia hali itakayowezesha pia kupunguza uharibifu na misitu ambapo amempongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa Nishati Safi ya Kupikia Duniani.
Veronica Nduva, Katibu Mtendaji Jumuiya ya Afrika Mashariki amepongeza Tanzania kuendesha mkutano huo kwa mafanikio na kueleza kuwa unaendana na malengo ya Jumuiya ya EAC ya kuhakikisha kunakuwa na uendelezaji wa rasilimali za Mafuta na Gesi Asilia unaozingatia utunzaji wa mazingira.