
Serikali imesema kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa katika sekta ya afya nchini unakwenda kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha Tiba Utalii kwa kutoa huduma za Afya kwa wagonjwa maalumu wa ndani na nje ya nchi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu, baada ya kufungua mradi wa kliniki mpya ya wagonjwa maalum na wa kimataifa iliyopo katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), itakayotoa huduma za kliniki kwa wagonjwa wa ndani na nje ya nchi, ambapo amebainisha kuwa kutokana na uwekezaji katika miundombinu, vifaa tiba na wataalamu, MOI imefanikiwa kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi ambapo hadi sasa 99% ya huduma za mifupa pamoja na 97% ya huduma za kibingwa za ubongo, mgongo na mishipa ya gahamu zinapatikana hapa nchini.
.
Pia, Waziri Ummy ametoa maelekezo kwa Hospitali nyingine kuwa na huduma za haraka, kwani Watanzania wanataka huduma za haraka na zilizo bora kwa kuzingatia weledi, maadili na taaluma wakati wa kumhudumia mgonjwa.

Aidha, Ummy amewataka Watanzania kuzingatia ulaji bora ikiwemo kupunguza matumizi ya sukari nyingi, chumvi nyingi pamoja na mafuta mengi ili kuepuka Magonjwa Yasiyoambukiza ikiwemo shinikizo la juu la Damu (Presha) na Kisukari kwa kuwa magonjwa hayo yamekuwa yakiongezeka Tanzania.
