Back to top

Ukarabati wa jengo la OPD katika zahanati ya Nyamainza wamalizika.

13 September 2018
Share

Serikali ya Canada kupitia mradi wake wa mama na mtoto imekamilisha ukarabati na upanuzi wa jengo la wagonjwa wa nje katika zahanati ya Nyamainza inayohudumia zaidi ya wakazi 16,000 wa vijiji vitano vya kata ya Gulumungu wilayani Misungwi mkoani Mwanza, ikiwa ni jitihada za serikali na wadau wa afya katika kutekeleza sera ya wizara ya afya ya kupunguza vifo vya mama na mtoto kabla na baada ya kujifungua katika maeneo ya vijijini.

 Meneja wa mradi wa mama na mtoto Tanya Salewski, akikabidhi jengo hilo amesema limekarabatiwa na kupauliwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 50 ili kuunga mkono jitihada za serikali za kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya nchini.
 
Baadhi ya wakazi wa kata hiyo ya Gulumungu wamesema hatua hiyo imewaondolea adha ya kutumia jengo chakavu.

Mganga mfawidhi wa zahanati hiyo ya Nyamainza, Bw. Bukumbi Maduka amesema kukamilika kwa ukarabati wa jengo hilo kutaimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wagonjwa wa nje.

Jengo la wagonjwa wa nje katika zahanati ya Nyamainza limekabidhiwa kwa kaimu mganga mkuu wa wilaya ya Misungwi Dkt.John Nyorobi ambaye amesema uwepo wa mradi huo katika wilaya ya Misungwi umewezesha kuboresha mfumo wa huduma za afya kwa ngazi ya zahanati kwa mama mjamzito kupata huduma bora.