
Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM amewashukuru wanachama na Viongozi waliokuwa chama CHAUMMA na CUF waliohamia Chama Cha Mapinduzi CCM akiwakaribisha wale wote wenye kukereka na kupoteza matumaini huko waliko.
"Kwa dhati kabisa niwashukuru ndugu zangu wote walioungana nasi leo, kilichovutia zaidi ni mama amemwambia baba hakuna matumaini huko, twende huku na wote wamehamia pamoja CCM. Wale wengine ambao bado wana roho za kukereketwa tuungane Tanzania yetu twende nayo kwa salama na utulivu." Amesema Dkt. Samia.
Dkt. Samia ametoa kauli hiyo leo kwenye Uwanja wa Ilulu, Lindi Mjini Mkoani Lindi wakati akizungumza na maelfu ya wananchi wa Mji huo wakati wa kuomba kura kwa wananchi wa eneo hilo, mara baada ya waliokuwa watia nia na wagombea Ubunge wa Vyama vya upinzani kutangaza kuhamia CCM na kupokelewa na Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dkt. Asharose Migiro.
Dkt. Samia pia ametumia fursa hiyo kueleza mafanikio makubwa ya serikali yake ya awamu ya sita, akisema hakuna awamu itakayosema imemaliza kazi zote lakini ndani ya miaka yake minne kazi kubwa imefanyika, akiahidi kuendelea na usambazaji wa umeme kwenye nusu ya Vitongoji vilivyosalia nchini pamoja na upelekaji wa huduma nyingine muhimu kwa wananchi ikiwemo huduma za maji, afya na elimu.
Mapema kwenye mkutano huo wa kampeni za Dkt. Samia, aliyekuwa Mgombea Ubunge Jimbo la Mchinga kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 kupitia Chama Cha CHAUMMA Bw. Yusuph Issa Tamba pamoja na Salum Baruan, Mbunge wa zamani kupitia CUF na Makamu mwenyekiti wa zamani wa Chadema Kanda ya Kusini kwasasa akiwa ni Mwenyekiti wa Jimbo la Lindi Mjini Chadema pamoja na Rehema Muhema, Mjumbe wa Baraza kuu la Uongozi Chama cha wananchi CUF pamoja na wanachama wengine wa Chadema na CUF walipokelewa ndani ya CCM na Balozi Dkt. Migiro.