Back to top

WAZIRI BASHE:SEKTA YA KILIMO KUONGEZA AJIRA ZENYE STAHA.

02 May 2024
Share

Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe amesema wizara yake  itaendelea kuwezesha upatikanaji wa ajira zenye staha na ushiriki wa vijana na wanawake kwenye kilimo kupitia utekelezaji wa Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (Building a Better Tomorrow – BBT).

"Wizara imeendelea kutekeleza programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) kwa vijana na wanawake yenye malengo ya kuongeza ajira zenye staha, kuongeza tija, kubakiza wakulima katika sekta na kupunguza umaskini," -  Waziri wa Kilimo Mh.Hussein Bashe.

Ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake,  ambapo amesema wizara itaanza kutekeleza mradi wa BBT katika halmashauri 100 zitakazotenga maeneo yenye ukubwa wa hekta 200 kwa kila halmashauri na kujenga miundombinu ya umwagiliaji katika maeneo hayo.

Aidha amesema Programu hiyo inatekelezwa kupitia miradi mikuu minne, ambayo ni kuwezesha upatikanaji wa ardhi ya kilimo na uanzishaji wa mashamba makubwa ya pamoja (Block farms) na umilikishaji wa ardhi, kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa vijana na wanawake (BBT - Mitaji), kuimarisha Huduma za Ugani (BBT – Ugani) na kuwezesha upatikanaji wa miundombinu ya umwagiliaji kwa wakulima wadogo (BBT – Visima).