
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeteketeza jumla ya kilogramu 4,402.02 za dawa za kulevya katika kiwanda cha saruji cha Twiga, kilichopo Wazo, jijini Dar es Salaam. Dawa zilizoteketezwa ni pamoja na kilogramu 2,168.18 za methamphetamine, kilogramu 1,064.29 za heroin, gramu 326.95 za cocaine, kilogramu 515.48 za bangi na kilogramu 653.74 za mirungi.
Dawa hizo zilihifadhiwa kama vielelezo vya mashauri mbalimbali yaliyopo mahakamani, ambapo baadhi ya mashauri bado yanaendelea kusikilizwa huku mengine yakiwa tayari yametolewa hukumu. Kwa mashauri ambayo bado hayajakamilika, Mahakama iliagiza dawa hizo kuteketezwa kutokana na hatari ya kuharibika au kubadilika umbo, kama Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka 2015 inavyotaka vielelezo vya dawa za kulevya kuharibiwa wakati shauri likiendelea au baada ya hukumu kutolewa.
Miongoni mwa mashauri yanayohusiana na dawa zilizoteketezwa ni kesi ya Najim Abdallah Mohamed iliyohusisha heroin kilogramu 882.71 na methamphetamine kilogramu 2,167.29. Aidha, mashauri yaliyotolewa hukumu ni Pamoja na ya Hassan Azizi aliyepatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha, Salum Shaaban Mpangula aliyehukumiwa kifungo cha maisha, Hemed Juma Mrisho maarufu kwa jina la “Hororo” aliyehukumiwa kifungo cha maisha, Ramadhan Shaban Gumbo aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, Irene Dickson Mseluka aliyehukumiwa miaka mitano jela na Gema Victor Mmasy aliyehukumiwa miaka mitatu jela.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kisheria na kiutendaji kuhakikisha Tanzania inalindwa dhidi ya madhara ya dawa za kulevya. Sambamba na hatua hizo, Mamlaka itaendelea kuutaarifu Umma kuhusu taarifa zinazohusu dawa za kulevya na kuimarisha ushirikiano na wananchi katika mapambano haya.