
Hali ya upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam imeimarika kufuatia kukamilika kwa marekebisho ya mtambo mmoja katika mitambo ya kuzalisha maji katika eneo la Ruvu chini huku kiwango cha maji katika Mto Ruvu kikitajwa kuwa ni mita 167 ikiwa ni zaidi ya kiwango cha kawaida hali inayotoa uhakika wa uzalishaji wa maji.
Akizungumza na wanahabari Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (DAWASA), Mhandisi Mkama Bwire, amesema wananchi hawapaswi kuwa na hofu kutokana na hali ya maji kuendelea kuimarika ikilinganishwa na wiki chache nyuma ambapo pia baadhi ya maeneo ambayo yalikosa maji yameanza kupata ikiwemo maeneo ya Tabata, Kinyerezi, Mbezi Makabe na maeneo ya Mshikamano.
Kwa upande wake Meneja Uzalishaji Mtambo wa Maji Ruvu Juu Mhandisi Juma Kasekwa, amesema marekebisho yaliofanywa ni katika pump na kuufanya mtambo wa Ruvu Juu kuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 196 kutoka lita milioni 122 kabla ya matengenezo.
Naye Everlasting Lyaro amezungumzia clip ya video ambayo imesambaa mtandaoni juu ya hali ya maji katika Mto Ruvu ambapo amesema si ya kweli na imelenga kuleta taharuki kwani maji yapo ya kutosha na uzalishaji ni mkubwa.